2 MAR AT 20:33

Sinalo jembe kamili, hani nina kiserema,
Siwezi stahimili, miale ikiterema,
Tatiza kiwiliwili, kunyanyua nimekoma,
Muda mrefu kulima, Swezi nina kiserema.

Sikulima jumapili, mwenzio naungama,
Nilogopa jua kali, lilonikatiza tama,
Shamba lenyewe maili, linahitaji hekima,
Muda mrefu kulima, swezi nina kiserema.

Sasa majuma mawili, vibayabaya nalima,
Sitoweza shamba hili, ni ukweli ninasema,
Ukubwa sitakabili, nateseka kuinama,
Muda mrefu kulima, Swezi nina kiserema.

Mara nyingi nimefeli, pekeangu nikilima,
Nakuacha pilipili, hamu kama inahama,
Unasonga mbalimbali, mato umeweka pima,
Muda mrefu kulima, Swezi nina kiserema.

Heri waite amali, walobobea kulima,
Wana nyingi staili, utaacha kulalama,
Afya yangu ninajali, sitaki mie nakama
Muda mrefu kulima, Swezi nina kiserema.

Shambani siwe bahili, faidi jamii nzima,
Jina liweke faili, kila mmoja apima,
Walo wasio adili, shamba sione huruma,
Muda mrefu kulima, Swezi nina kiserema.


|NINA KISEREMA|

- 𝕃𝕦𝕓𝕒𝕟𝕘𝕒